Baada ya kusota gerezani kwa miaka 13 na miezi minne, wakitumikia
kifungo cha maisha, hatimaye mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi
nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanae, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’
jana walirejea uraiani kwa msamaha wa Rais John Pombe Magufuli
Babu Seya na na Papii Kocha walitoka katika Gereza la Ukonga saa 12 jioni huku wakishangiliwa na mashabiki pamoja na ndugu zao.
Babu Seya aliyekuwa akipunga mkono akionekana kutoamini kilichotokea
alivaa mavazi kitanashati kama ilivyokuwa kwa Papii Kocha ambaye alikuwa
akipunga mkono huku akitabasamu na kuzungumza na mashabiki wake.
Pamoja na kuwa wameachiwa lakini haya ndiyo waliyopitia wanamuziki
hao katika safari yao kuanzia kushtakiwa mpaka kuhukumiwa na kuachiwa
huru.
Mwanzo wa kesi
Safari ya wanamuziki hao ya kuishi maisha ya gerezani ilianza baada ya
kutiwa mbaroni na kisha kufunguliwa kesi ya jinai wakikabiliwa na
mashtaka ya ubakaji na ulawiti, wakituhumiwa kuwabaka na kuwalawiti
watoto 10 wa kike wenye umri kati ya miaka 6 na 8 ambao walikuwa ni
wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza jijini Dar es Salaam.
Oktoba 12, 2003: Watiwa mbaroni
Babu Seya na wanae watatu walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na
kufikishwa kituo cha Polisi cha Magomeni jijini Dar es Salaam,
wakikabiliwa na tuhuma hizo za ubakaji na ulawiti wa watoto wa kike
wenye umri wa chini ya miaka 10.
Waliotiwa mbaroni walikuwa ni Nguza mwenyewe, Papii Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza ambao wote ni watoto wake.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi hiyo mahakamani, Babu Seya na wanae
walitiwa mbaroni baada ya mmoja wa watoto hao ambao walikuwa ni
wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, kugunduliwa na bibi yake kuwa
alikuwa ameharibiwa sehemu zake za siri.
Baada ya bibi huyo kumhoji mtoto huyo ndipo alipoeleza kuwa amekuwa
akifanyiwa vitendo hivyo na Babu Seya na kwamba si yeye pekee bali wapo
na wenzake ambao nao hufanyiwa hivyo, huku akiwataja kwa majina.
Kutokana na taarifa hizo ndipo bibi huyo alipotoa taarifa kwenye vyombo vya dola na hatimaye watuhumiwa kutiwa mbaroni.
Oktoba 16, 2003: Wapandishwa kizimbani
Siku nne baadaye baada ya kutiwa mbaroni, Babu Seya na wanae hao watatu
pamoja na mwalimu wa kike wa Shule ya Msingi Mashujaa walipandishwa
kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mahakamani hapo walisomewa jumla ya mshtaka 21, mashtaka 10 ya ubakaji
wa watoto hao na mashtaka mengine 11 ya kuwanajisi watoto hao.
Juni 25, 2004: Kifungo cha maisha jela
Baada ya kuwa wamesota mahabusu wakati kesi yao ikiendelea kusikilizwa,
hatimaye Juni 25, 2004 walianza maisha mapya baada ya Mahakama ya Kisutu
kuwahukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Addy
Lyamuya baada ya kuwatia hatiani kwa makosa 20 ya kuwabaka na kuwalawiti
watoto hao.
Pamoja na adhabu hiyo ya kifungo, pia Hakimu Lyamuya aliwaamuru kuwalipa fidia ya Sh2 milioni watoto hao kila mmoja.
Wakati Babu Seya na wanaye wakitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo, mshtakiwa wa tano, mwalimu wa shule hiyo aliachiwa huru.
Januari 27, 2005: Ukuta rufaa ya kwanza
Harakati za wafungwa hao kujinasua katika adhabu hiyo zilianza mara moja
baada ya hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu ambapo kupitia kwa wakili
wao aliyewatetea katika kesi ya msingi, Hubert Nyange walikata rufaa
Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Januari 27, 2005 waligonga ukuta baada ya Jaji Thomas Mihayo aliyesikiliza rufaa yao hiyo kutupilia mbali.
Februari 11, 2010: Babu Seya, Papii Kocha wang’ang’aniwa, wenzao waachiwa
Kwa mara nyingine, Babu Seya na wanae mara hii wakiwakilishwa na Wakili
Mabere Marando, walikata rufaa Mahakama ya Rufani wakipinga hukumu ya
Mahakama Kuu.
Hata hivyo, matumaini ya Babu Seya na Papii Kocha kurudi uraiani kwa
mara nyingine yalitoweka baada ya kushindwa katika rufaa yao ya pili.
Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyoandaliwa na jopo la majaji
watatu; Nathalia Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk, Februari 11,
2010 ilitupilia mbali rufaa dhidi yao kuwa hoja zao hazikuwa na mashiko
na hivyo ikaridhia kuendelea na kifungo hicho cha maisha.
Wakati mahakama hiyo ikiridhia Babu Seya na Papii Kocha kuendelea na
kifungo chao, iliwaachia huru Mbangu na Francis ikikubaliana na hoja za
Wakili Marando kuwa hapakuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani.
Desemba 22, 2013: Wakwama tena
Licha ya Mahakama ya Rufani kuwang’ang’ania na kuridhia kuendelea na
adhabu hiyo, Babu Seya na Papii Kocha hawakukata tamaa kupambana kuwa
huru.
Kwa mara nyingine, walifungua maombi ya marejeo wakiiomba mahakama
hiyo irejee tena hukumu yake hiyo na hatimaye ione kuwa ilikosea na
hivyo iwaachie huru.
Hata hivyo, mara hii tena waligonga ukuta baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yao kuwa hayana mashiko ya kisheria.
Katika uamuzi wake uliosomwa na kaimu msajili, Zahra Maruma, Mahakama
ya Rufani ilitupilia mbali maombi hayo ikisema kuwa waomba marejeo hao
hawakuwa na hoja za msingi.
Ilisema hoja zilizotolewa katika maombi hayo ya marejeo si tu kwamba
hazikidhi kuifanya irejee hukumu hiyo, bali pia hoja hizo zilishatolewa
wakati wa usikilizwaji wa rufaa na kutolewa uamuzi.
Wenyewe watoa kauli
Akisindikizwa na askari kuelekea kwenye gari kurejeshwa gerezani,
Papii Kocha alisema: “Sasa tunamuachia tu Rais ndiye anayeweza kutoa
uamuzi wa mwisho.”
Lakini Babu Seya kwa upande wake, baada ya kupanda katika gari hilo
tayari kurejea gerezani alisema bila ya kufafanua: “Kwa binadamu ni
makosa, lakini kwa Mungu hakuna makosa.”
Juni 21, 2014: Wamlilia JK awasamehe
Baada ya kuona kuwa harakati zao mahakamani zimeshindikana, Babu Seya na
mwanaye Papii Kocha waliamua kumwangukia Rais Jakaya Kikwete wakimuomba
awasamehe na kuamuru waachiwe huru.
Walitoa ombi hilo kupitia wimbo wao wakati wakitumbuiza katika
maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga,
Dar es Salaam mbele ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Babu Seya na Papi Kocha walitumbuiza wakiwa na bendi ya wafungwa na
katika wimbo huo walimuomba Waziri Chikawe kufikisha ombi lao kwa Rais
Kikwete.
“Waziri Chikawe tunaomba umfikishie Rais Jakaya Kikwete ombi letu,
mwambie atusamehe. Hata Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini Yesu
alimsamehe kwa nini sisi…,” alisikika akiimba Papii Kocha.
Akijibu ombi hilo wakati akiwahutubia wananchi Waziri Chikawe alisema:
“Nimesikia maombi yenu, yamefika na nitajitahidi kuyafikisha kwa Rais
Kikwete.”
Novemba 2015: Watua Mahakama ya Haki za Binadamu
Baada ya harakati zao kushindwa katika mahakama za ndani ya nchi, Babu
Seya na mwanae waliamua kuendelea na mapambano hayo katika mahakama za
nje.
Mara hii walitua katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR)
ambako walifungua kesi namba 006/2015, wakidai kuwa haki zao zilivunjwa,
hivyo walikuwa wakiiomba iwaachie huru.
Miongoni mwa hoja za walalamikaji hao zilizowasilishwa mahakamani hapo
ni pamoja na kwamba mwenendo wa shauri lao la msingi haukufanyika kwa
kuzingatia haki.
Vilevile, walidai kuwa hati ya mashtaka dhidi yao ilikosewa kuandikwa
tarehe ambayo tuhuma za makosa yao zilidaiwa kufanywa hivyo wakashindwa
kutayarisha utetezi wao na kwamba mahakama iliyowatia hatiani
ilijielekeza katika ushahidi wa upande wa mashtaka pekee usioshirikisha
ushahidi mwingine.
Walikuwa wakidai kuwa Serikali kupitia maofisa wake, ilivunja misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa.
No comments:
Post a Comment