Straika Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani.
LONDON, England
ARSENAL chini ya kocha wake Arsene Wenger inapambana kuhakikisha
inamsajili straika Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Borussia Dortmund ya
Ujerumani.
Aubameyang raia wa Gabon anatakiwa na Arsenal kwa udi na uvumba ili
kuziba nafasi ya straika Alexis Sanchez ambaye anatarajiwa kujiunga na
Manchester United au Manchester City.
Maisha ya Aubameyang katika Klabu ya Borussia Dortmund sasa siyo
mazuri na inaonekana wazi straika huyo anataka kuondoka na klabu
iliyoonyesha nia ya kumsajili ni Arsenal.
Wenger hana jinsi zaidi ya kumuachia Sanchez kwenda jijini Manchester
kwani isipofanya hivyo sasa, inaweza kumtoa bure katika usajili ujao
kabla ya msimu mpya.
Hata hivyo zipo sababu zinazoonyesha kuwa, Aubameyang anaweza kuisumbua Arsenal kutokana na sababu zifuatazo:
#5 Kulazimisha ushindi
Aubameyang anajua kufunga na akiwa karibu na lango ni mtu hatari sana
kwa wapinzani. Hata hivyo, ana tatizo la kutokuwa mpambanaji kwa ajili
ya timu na hana njia nyingi za kuwabuguzi mabeki, akishindwa njia moja
ndiyo basi tena. Anategemea kufunga kwa kutengenezewa nafasi na
wakishindwa kumfanyia hivyo ndiyo basi tena.
#4 Tatizo la ulinzi
Moja kati ya matatizo makubwa ya Aubameyang awapo uwanjani ni mchango
wake wa kukaba. Kwa soka la sasa hasa England, kukaba ni kazi ya
mshambuliaji pia ili kupunguza kasi ya adui. Sasa Aubameyang yeye si
mzuri katika kukaba hivyo atapata tabu katika mfumo huo.
#3 Hayupo kama zamani
Aubameyang wa sasa si yule wa msimu mmoja au miwili nyuma, ameshuka
pia vituko vyake nje ya uwanja ni tatizo kichwani mwake. Sawa, sasa
anaweza kuwa amefunga mabao 21 katika mechi 23 msimu huu, lakini
hailingani na nafasi anazopoteza uwanjani sasa katika kikosi cha
Borussia Dortmund.
#2 Gharama yake haiendani na umri
Aubameyang sasa ana umri wa miaka 28, hivyo dau la Borussia Dortmund
la kumuuza kwa pauni milioni 53 (Sh bilioni 162.8), haiwezi kuwa na
faida kwao kwani hatoweza kucheza kwa ushindani kwa muda mrefu. Hii ina
maana kuwa, Arsenal haitaweza kumtumia kwa muda mrefu.
#1 Hawezi kuwa Alexis Sanchez
Ukweli ni kwamba, Aubameyang hawezi kuwa mbadala sahihi wa Alexis
Sanchez. Arsenal inadhani Aubameyang ndiye mbadala sahihi wa Sanchez
lakini ukweli ni kwamba wawili hao wapo tofauti kabisa. Aubameyang
anacheza kwa mtindo mmoja na kwa kutumia upande mmoja tu lakini Sanchez
yupo pande zote. Hapa ndipo Arsenal inapoongeza nguvu pia kumnasa Malcom
wa Bordeaux.