YANGA
SC itapanda boti kurejea mjini Dar es Salaam kesho baada ya kutolewa
kwenye michuano ya Kombe la Mapunduzi kwa penalti 5-4 na URA ya Uganda
kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 jioni ya leo Uwanja wa Amaan,
Zanzibar.
Yanga
SC imeendeleza utamaduni wake wa kufanya vibaya kwenye hatua ya matuta
baada ya mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa kumdakisha mpira kipa
wa URA, Alionzi Nafian.
Chirwa
alikosa penalti ya mwisho ya Yanga baada ya wenzake wote wanne, Mkongo
Papy Kabamba Tshishimbi na wazalendo Hassan Ramadhani Kessy, Raphael
Daudi Lothi na Gardiel Michael Mbaga kufunga.
Katika
mchezo huo uliochezeshwa na refa Issa Hajji, aliyesaidiwa na Shehe
Suleiman na Mwanahija Makame, penalti za URA zilifungwa na Patrick
Mbowa, Enock Kigumba, Shafiq Kagimu, Jimmy Kulaba na Brian Majwega.
Katika
dakika 90 za mchezo timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa URA
ndiyo walioonekana kulitia misukosuko zaidi lango la Yanga.
Tofauti
na ilivyotarajiwa kwamba kuingia kwa Chirwa kipindi cha pili kwenda
kuchukua nafasi ya Pius Buswita kungeiongezea nguvu safu ya ushambuliaji
ya Yanga, lakini Mzambia huyo alishindwa kucheza vizuri kutokana na
kile kilichoonekana wazi hakuwa fiti.
Chirwa
alikuwa kwao Zambia kufuatia mgomo wake wa kushinikiza alipwe fedha za
usajili na amerejea juzi Dar es Salaam na moja kwa moja kusafirishwa
kuletwa Zanzibar kabla ya kuingizwa uwanjani kipindi cha pili.
Na
hata penalti aliyokwenda kupiga ilikuwa ya ovyo kabisa na kipa wa URA
hakuhitaji kujisumbua kuiokoa, kwani mpira ulimkuta mikononi tena pale
pale aliposimama.
Nusu
Fainali ya pili inafuatia kati Azam FC na Singida United Saa 2:15 usiku
hapo hapo Uwanja wa Amaan na Fainali itachezwa Jumamosi.
Kikosi
cha URA kilikuwa; Alionzi Nafian, Enock Kibumba, Brian Majwega, Allan
Munaaba, Patrick Mbowa/Jimmy Kulaba dk92, Julius Mutyaba, Nicholas
Kagaba, Shafiq Kagimu, Bokota Labama/Peter Lwasa dk70, Kalama Deboss na
Charles Ssempa/Hudu Mbulikyi dk70.
Yanga
SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent,
Kelvin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita/Obrey Chirwa dk53,
Said Juma ‘Makapu’/Raphael Daudi dk92, Ibrahim Ajib, Juma Mahadhi/Yohann
Nkomola dk75 na Emmanuel Martin/Gardiel Michael dk85.
No comments:
Post a Comment