EMMANUEL Okwi amewaambia mashabiki wa Simba kwamba licha ya yeye
kutokuwa sehemu ya kikosi kwa sasa katika michuano ya Mapinduzi lakini
kwa jinsi alivyoona kwenye Azam TV hakuna ya kuwazuia kubeba ndoo.
Okwi
hatofautiani na Haruna Niyonzima ambae amepewa kazi pevu ya kujifua
bichi Jijini Dar es Salaam lakini anaamini kuwa kombe litakwenda Simba
kwavile sasa vijana wameamua kufanya kazi.
Okwi, mwenye mabao nane katika Ligi Kuu Bara, ameshindwa kuwa sehemu
ya wachezaji wa Simba wanaoshiriki Mapinduzi kutokana na kubaki kwao
Uganda ambako anaendelea na matibabu ya enka. Akizungumza na Spoti Xtra,
Okwi ambaye anasherehekea siku yake ya kuzaliwa Desemba 25 kila mwaka,
alisema; “Mimi sipo ndani ya timu kwa sasa lakini nikwambie tu kuwa bado
sijaona timu ambayo inaweza kuisimamisha Simba.”
“Nasema hivyo kwa sababu ukitazama wachezaji ambao wapo, wana viwango
vya hali ya juu sana na uzoefu mkubwa wa kufanya vyema katika michuano
hiyo, imani yangu ni kwamba Simba lazima wachukue ubingwa huo wa
Mapinduzi hata kama sipo,” alisema Okwi.
NIYONZIMA YUKO BICHI
Kocha wa Simba, Masoud Djuma amemwambia Haruna Niyonzima asibanduke
bichi kama anataka kuwa fiti na arudi kwenye kikosi chake. Niyonzima
aliyetua Simba katika usajili wa dirisha kubwa kwa dau la milioni 115
akitokea Yanga, kwa sasa ameshindwa kuwa sehemu ya kikosi hicho cha
Simba ambacho kinapigania ubingwa wa Mapinduzi ambayo inaendelea
visiwani Zanzibar kutokana na majeruhi.
“Kwa sasa kocha Masoud Djuma amenipangia programu maalumu ya kwenda
bichi na kufanya mazoezi huko tena nikiwa pekupeku kwa ajili ya
kujiimarisha tatizo la nyayo ambalo linanisumbua na kunifanya niwe nje
ya timu kule Zanzibar katika michuano ya Mapinduzi.
“Naamini hadi pale watakaporudi nitakuwa nimepona na kuwa tayari
kucheza kwa mara nyingine, kama siyo kocha Djuma basi kwa sasa ningekuwa
nacheza kwani watu wanaona kama siumwi vile lakini yeye ameliona hilo
na kunipa muda huu wa kupumzika na kufanya mazoezi kwa ajili ya kurejea
katika hali yangu ya zamani,” alisema Niyonzima.
No comments:
Post a Comment