Wednesday, January 10, 2018

TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA KAPERA

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha beki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Omary Kapera aliyefariki dunia juzi kuzikwa jana mchana.

Rais Karia amesema kwamba amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo; "Nimeshtushwa na taarifa hizo za kifo cha Kapera hasa ikichukuliwa bado tupo kwenye majonzi ya kumpoteza mchezaji mwingine wa zamani Athuman Juma Chama, kwa niaba ya Shirikisho natoa pole kwa wote walioguswa na msiba huo kuanzia kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki,”alisema Rais Karia.
Omar Kapera ‘Mwamba Kifua’ alikuwa sentahafu wa Yanga tangu miaka ya 1960 hadi 1977 alipokwenda kujiunga na Nyota Afrika ya Morogoro kufuatia mgogoro mkubwa uliobuka klabu ya Jangwani mwaka 1976.
Kapera na kundi la wachezaji wenzake walioondoka Yanga baada ya mgogoro huo wa kihistoria, baadaye walirejea Dar es Salaam kuasisi Pan Africans iliyokuja kuwa tishio pia katika soka ya Tanzania kabla ya kupoteza makali baada ya muongo mmoja

Kapera alikuwepo kwenye kikosi cha Yanga kilichoichapa Simba SC 5-0 Juni 1, mwaka 1968 Uwanja wa Karume, Dar es Salaam siku hiyo mabao ya wana Jangwani yakifungwa na Maulid Dilunga mawili dakika ya 18 kwa penalti na 43, Salehe Zimbwe dakika za 54 na 89 na Kitwana Manara ‘Popat’ dakika ya 86.
Na ni kikosi hicho kilichofika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili mfululizo mwaka 1969 na 1970 na kutolewa na Asante Kotoko ya Ghana mara zote 

No comments:

Post a Comment