WAZIRI
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe leo
amewatembelea wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa
miaka 17, Serengeti Boys waliopo kambini kwenye hostel za Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), zilizopo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Katika
ziara yake hiyo, Waziri Mwakyembe alijionea namna wachezaji hao
wanaoshi na kufanya mazoezi chini ya walimu wao, Mdenmark Kim Poulsen na
Msaidizi wake, Oscar Milambo.
Pamoja
na kuzungumza nao na kuwatia moyo ili wajitume zaidi, Waziri Mwakyembe
aliwaachia ujumbe wa Serikali wachezaji wa Serengeti Boys ambao wote
hawazidi umri wa miaka 16.
Dk.
Mwakyembe akitoa salamu za Serikali amewaambia vijana wanaounda timu
hiyo kuwa serikali yao inawaamini na wanalo jukumu la kuiperusha vyema
bendera ya Tanzania.
Amewataka
kupambana kwaajili ya Tanzania na kuhakikisha wanafanya vyema kwenye
kila mashindano huku akiwataka makocha wa kikosi hicho kuwapa mafunzo
mazuri kwa ustawi wa Vijana hao.
Aidha,
Dk. Mwakyembe amesema anaamini Vijana hao watakuwa bora chini ya TFF
iliyopo madarakani inayoongozwa na Rais Ndugu Wallace Karia.
"Naamini mtaimarika na kuwa bora maana hata TFF hii sasa ina ari na morali kubwa" amesema Dk. Mwakyembe.
Katika
ziara yake hiyo Dk. Mwakyembe alipata nafasi ya kutazama Serengeti Boys
ikiifunga 4-1 Makongo Sekondari katika mchezo wa kirafiki.
Kabla
ya mchezo huo Serengeti Boys walicheza mchezo mwingine wa kirafiki
dhidi ya Kituo cha Bombom na kutoa sare ya kufungana bao 1-1.
Wachezaji
34 wakiwemo 30 wa ndani na makipa wane, wapo kambini Serengeti Boys
tangu mwanzoni mwa mwezi hadi Januari 28, 2018 kwa maandalizi ya
michuano CECAFA Challenge U-17.
Maandalizi
hayo ya Serengeti Boys yatakwenda sambamba na kucheza mechi za kirafiki
kabla ya kuhairisha kambi hiyo itakayokuwa ikifanyika mara kwa mara na
mpango uliopo ni kila mwezi timu hiyo kuingia kambini.
No comments:
Post a Comment