Kila mtu anakuwa na mawazo yake katika
jambo fulani, lakini kiungo nyota wa Simba, Shiza Kichuya anaweza
kutofautiana na wengi sana kuhusiana na Amissi Tambwe wa Yanga.
Kwa wale wanaoamini Tambwe anaweza
kuibuka na kufanya maajabu na mwisho kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu
Bara, Kichuya anasema "haiwezekani hata kidogo."
Tambwe ni majeruhi ingawa tayari ameanza
kufanya mazoezi mepesi na ligi inakwenda mechi ya 10 kwa kila timu
katika mechi za leo na kesho.
Mshambuliaji huyo Mrundi hakuwahi
kucheza hata mechi moja katika msimu huu na tayari aliwahi kuwa mfungaji
bora mara mbili na mfungaji katika nafasi ya pili mara moja, hiyo ni
katika misimu minne aliyocheza ligi hiyo.
Hadi sasa imeshapita michezo tisa ya ligi kuu huku wikiendi hii ikitarajiwa kupigwa kwa kumi, ambapo hadi sasa Tambwe hajafunga hata bao moja pia hajacheza hata mechi moja akiuguza jeraha la goti.
“Unajua kwa sasa ushindani umekuwa mkubwa sana kwa washambuliaji ambapo kila mmoja anakitolea macho kiatu cha ufungaji bora, kila mtu anajitahidi kufunga ili aweze kulifanikisha suala hilo.
“Ni ngumu kwa Tambwe kuwa mfungaji bora kwa sababu ameshakosa mechi tisa kwa sababu ya majeraha na hata akirejea haitakuwa rahisi kutukuta kwenye idadi hii ya mabao.
“Akirudi uwanjani, Tambwe atahitaji siku kadhaa za kurudisha makali yake sasa hapo na sisi tutakuwa tunapambana tufunge zaidi kwa hali hii naona haitakuwa rahisi awe mfungaji bora,” alisema Kichuya.
No comments:
Post a Comment