Saturday, November 11, 2017

WACHEZAJI VPL HATARINI KUTEMWA HEROES



Wachezaji wa timu ya Taifa ya Soka ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), ambao wanacheza ligi kuu Tanzania bara huenda waachwa katika kikosi hicho kutokana na kutopewa ruhusa na vilabu vyao kujiunga na timu hiyo ya Taifa mpaka ligi kuu bara itakapokwenda mapumziko.

Kocha mkuu wa Zanzibar Heroes Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema kutokana na kutopewa ruhusa wachezaji hao huenda wakaachwa badala yake wakaitwa wachezaji wengine wanaocheza soka visiwani Zanzibar.
Morocco amesema ikifika Novemba 15 ikiwa bado wachezaji hao hawajawasili kambi ya Heroes watalazimika kuachana nao na kuongeza nguvu kwa vijana wanaocheza vilabu vya Zanzibar kwani hawawezi kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na kambi siku chache kabla ya kusafiri.
“Tumeshaanza mazoezi tangu juzi, lakini uhakika wa kuwapata wachezaji wanaocheza ligi ya bara ni ngumu, tumewasiliana na vilabu vyao lakini wametuambia wachezaji hawatowaruhusu kujiunga na sisi mpaka ligi isimame Novemba 19.”
“Sisi tunataka kuondoka Novemba 22, hawatopata mufa wa kukaa na wenzao kwa sababu huenda wakafika Zenj Novemba 20 au 21 sasa hapo bora tuwaache tuite wengine wanaocheza hapahapa Zanzibar.”
Wachezaji waliyoitwa awali katika kikosi cha Zanzibar Heroes ambao wanatoka ligi kuu Tanzania bara ni walinzi Abdallah Haji “Ninja” (Yanga), Adeyum Saleh ‘Machupa’ (Kagera Sugar), Haji Mwinyi Ngwali (Yanga), Abdulla Kheir ‘Sebo’ (Azam), Viungo Mudathir Yahya (Singida United), Mohd Issa ‘Banka’ (Mtibwa Sugar) na Suleiman Kassim ‘Seleembe’, (Majimaji) pamoja na washambuliaji Kassim Suleiman (Prisons), Matteo Anton (Yanga) na Seif Rashid Abdallah ‘Karihe’ (Lipuli).
Wakati huohuo Mlinzi kinda wa Zanzibar Heroes aliyeitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho Ibrahim Abdallah wa Taifa ya Jang’ombe amepania kupigana kufa au kupona ili apate nafasi ya kwenda nchini Kenya katika Mashindano ya CECAFA Chalenji CUP yanayotarajiwa kufanyika Novemba 25 na kumalizika Disemba 9 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment