![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjFS8JGyBklt1CpbBEZNAxabsaM_hBaLv9ryekprmzNKiJnOJZXECj29Rh_oKtkkdN_yKlWQEhx2fY84bSAXO712v56JOjaBNIdfM6g0rgC96-mxeB2nR5eGaa_c_bI6WbPMLXTmupLTHIM/s400/1.jpg)
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Hebron Mwakagenda amesema wameazimia kufungua kesi ya kudai haki ya kufanya maandamano ya amani nchini baada ya maandamano yao yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Oktoba 30, mwaka huu kuzuiliwa na Jeshi la Polisi.
Mwakagenda
amesema Oktoba 7, mwaka huu walitoa tamko kwa umma la kukusudia kufanya
maandamano ya amani nchi nzima kumpongeza na kuunga mkono juhudi za
Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusimamia rasilimali za taifa pamoja
na kupiga vita rushwa lakini Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam liliwazuia.
Pia
maandamano hayo yalilenga kufikisha ujumbe kuhusu haja ya serikali
kurejesha mchakato wa katiba mpya ili taifa liweze kupata katiba mpya
chini ya uongozi wa Rais Magufuli lakini jitihada zao ziligonga mwamba.
“Kwa
uzito huu JUKATA tulimwandikia Rais Magufuli ili ayapokee maandamano
hayo ambayo yalikuwa yamepangwa kuanzia ofisi zetu zilizopo Mwenge hadi
Viwanja vya Mnazi Mmoja, hadi leo hatujapata majibu ya barua iliyotumwa
Ikulu kwa Rais Magufuli juu ya ombi letu. Lakini tulipokea barua kutoka
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ikikataza kufanyika kwa
maandamano hayo ya c amani,” amesema Mwakagenda.
Jeshi
la Polisi lilizuia maandamano hayo kwa sababu tatu, zikiwemo kwamba
Rais Magufuli hakuthibitisha kushiriki kwenye maandamano hayo, kufanya
maandamano umbali mrefu kutoka Mwenge hadi Mnazi Mmoja kutaathiri
shughuli kwa kufunga barabara na Oktoba 30 ndiyo siku ambayo mitihani ya
kidato cha nne ingekuwa ikifanyika.
“Kwa
sababu hizi zilizotumika kukataza maandamano, tumefikia maamuzi ya
kwenda kufungua kesi mahakamani kudai haki ambayo inaminywa na
kukandamizwa na Jeshi la Polisi kwa kutumia sababu nyepesi.
“Tupo
kwenye hatua za mwisho kutekeleza uamuzi huu na kwamba jopo la mawakili
wasomi wasiopungua kumi wakiongozwa na Dkt. Rugemeleza Nshala
watahusika katika mchakato huu wa kudai mahakamani haki hii ya kufanya
maandamano ya amani,” alifafanua.
Mwakagenda
alihitimisha kwa kusema Tanzania inafuata misingi ya kidemokrasia na
utawala wa sheria ambapo misingi mikuu ya kidemokrasia ni pamoja na
uhuru wa watu kukusanyika na kujadiliana kwa mujibu wa sheria kujadili
masuala yanayohusu taifa.
No comments:
Post a Comment