TIMU
ya soka ya taifa ya Senegal imekata tiketi ya fainali za kombe la Dunia
mwakani nchini Urusi baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji,
Afrika Kusini Uwanja wa Peter Mokaba mjini Polokwane jana.
Mabao
ya Senegal yalifungwa na mshambuliaji wa West Ham, Diafra Sakho dakika
ya 12 na Thamsanqa Mkhize aliyejifunga dakika ya 38.
Ikumbukwe
huo ulikuwa mchezo wa marudio, baada ya ushindi wa 2-1 wa Bafana Bafana
Novemba 12 mwaka jana kutenguliwa na kuamriwa mechi irudiwe, kufuatia
refa Joseph Lamptey kufungiwa maisha na Mahakama ya Usuluhishi (CAS).
FIFA
ilimkuta na hatia Lamptey ya kupanga matokeo ili kuibeba Afrika Kusini,
ambayo sasa italazimika kushinda mechi zake mbili za mwisho za kufuzu
ili kuungana na Simba Teranga.
Mshambuliaji
wa Liverpool, Sadio Mane ndiye aliyetoa pasi ya bao lililofungwa na
Sakho na Senegal inakuwa nchi ya tatu ya Afrika kujihakikishia tiketi ya
Urusi mwakani, baada ya Misri na Nigeria kuwa za kwanza kufuzu.
No comments:
Post a Comment