Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo.
………………………………………………………………
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Mhe. Selemani Jafo
ameagiza mikoa yote kuanza Kampeni kabambe iitwayo ‘Kiwanda changu Mkoa
wangu’ ili kuharakisha maendeleo na kuongeza upatikanaji wa ajira kwenye
maeneo hayo.
Jafo ametoa maagizo hayo ya
wizara yake kwa Wakuu wa mikoa yote ya Tanzania bara wakati alipokuwa
akizungumza na Wakuu wa mikoa sita wapya walioapishwa leo na Rais
Dk.John Magufuli.
Akizungumza na Wakuu hao baada ya
kukamilisha kwa zoezi la kiapo, Jafo amesema kampeni hiyo inatarajiwa
kuzinduliwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka huu.
Amesema Mpango huo kabambe ni wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati katika mamlaka za serikali za mitaa.
“Hii sasa ni changamoto kwenu
wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya hapa nchini nataka kila mkoa ujenge
angalau viwanda 100 kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Desemba 2017
hadi Desemba 2018,”anasema jafo
Amebainisha malengo yake ni
kwamba ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja zaidi ya viwanda vidogo na
vya kati 2600 viwe vimejengwa nchini.
Katika kufanikisha mpango huo,
Waziri Jafo amewataka maafisa wa maendeleo ya jamii kufanya kazi ya
kuviunganisha vikundi vilivyopo katika halmashauri zao ili viweze kupata
fursa za mifuko mbalimbali ya uwezeshaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri
mkuu na fedha za uwezeshaji vijana na wanawake katika halmashauri zao.
Kampeni hiyo endapo itafanikiwa basi itakuwa ni mchango mkubwa kutoka wizara ya TAMISEMI katika ajenda ya viwanda hapa nchini.