Mwaka 1984 Tottenham Hotspur walikuwa na kocha aitwaye Keith Burkinshaw lakini mwaka huo huo Burkinshaw alibwaga manyanga, baada ya kuachia ngazi ilibidi Tottenham waanze kutafuta kocha mpya
.
Mwenyekiti wa Tottenham Hotspur kwa wakati huo Irving Scholar alimuona kocha wa Aberdeen Fc aitwaye Alex Ferguson kama mtu sahihi kwa ajili ya kuchukua mikoba ya Keith Burkinshaw.
Scholar alianza maongezi na Ferguson na inasemekana maongezi yalifikia pazuri, na wakati huo Scholara aliamini kwamba ukifanya makubaliano na mtu mkapeana mkono baasi atakuwa amekubali ombi lako na Fergie alimpa mkono.
Scholar alifurahia jinsi Fergie alivyolipokea ombi lake na mazungumzo kuhusu mkataba wa Ferguson kuifundisha Tottenham yakawa yanaelekea ukingoni kwa imani kubwa kwamba Fergie anapewa timu.
Scholar alimchukua mjumbe wa bodi ya Tottenham kwa ajili ya kwenda kumaliza kila kitu na Fergie na kikao cha mwisho kilikuwa kifanyike uwanja wa ndege na wote wakafika akiwemo Ferguson.
Scholar alimuuliza Fergie kama yuko tayari? Ferguson akamuambia yupo tayari na wakapeana mikono lakini Ferguson hakuwa na raha wakati wakipeana mikono ndipo Scholar akajua kuna kitu hakipo sawa.
Ferguson hakusema nini hakipo sawa na wote wakaondoka huku Fergie akaenda zake kuendelea kuifundisha Aberdeen na mwaka 1986 kocha huyo alijiunga na klabu ya Manchester United.
Manchester United klabu ya zamani ya Alex Ferguson mwishoni mwa wiki hii wataikabili Liverpool, lakini kama ilivyo kwa hadithi ya Ferguson kuna nyota wa zamani wa klabu hiyo ambaye almanusra akipige Liverpool.
Kocha wa zamani wa Liverpool Graume Souness alishauriwa kumnunua mshambuliaji wa zamani wa Manchester United Eric Cantona pamoja na kipa wa zamani wa Manchester United Peter Schmeichel lakini akawatosa.
Souness anasema alimjua Cantona kupitia Michel Platini lakini wakati wa mazungumzo kati yake na Platini ndipo Platini akamshauri kuhusu Eric Cantona akimuambia ni mchezaji mzuri lakini mwenye matatizo.
Souness hakuhitaji wachezaji wakorofi kwa kipindi hicho na moja kwa moja akamuambia Platini kwamba angehitaji mchezaji mzuri lakini sio mchezaji mkorofi wala mwenye shida nje ya uwanja hivyo hamtaki Cantona.
Kuhusu Schmeichel kocha Souness alikuwa tayari ana makipa wawili hivyo hakuhitaji kuongeza mwingine, Ferguson, Cantona na Schmeichel tangu walipojiunga na United kilichofuata imekuwa ni historia.
No comments:
Post a Comment