WACHEZAJI wa Simba kwa pamoja wamelazimika kumfuata kocha wao Joseph
Omog na kumsihi ampange kikosi cha kwanza John Bocco katika mchezo wa
leo dhidi ya Yanga.
Yanga inakairibisha Simba kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
katika mchezo namba 58 wa Ligi Kuu Bara ukiwa ni wa kwanza kwao kwa Dar
es Salaam msimu huu wa ligi.
Mmoja wa wachezaji wa Simba, aliliambia Championi Jumamosi kuwa,
ilibidi wamfuate kocha wao na kumuomba ampe nafasi Bocco katika kikosi
cha kwanza kwani ni mpambanaji anayewaweza Yanga.
“Tumemuomba kocha ampe nafasi Bocco kwani anaweza kupambana na mabeki
wa Yanga kama Yondani (Kelvin), unajua wanacheza kibabe sana sasa
ukimuweka mtu mwingine hatawaweza.
“Bocco hata akichezewa rafu huwa hakati tamaa, yeye anaenda tu na
mabeki watatumia muda mwingi kumzuia yeye huku sisi wengine tukiweka
sawa mipango ya ushindi.
“Kocha ametusikiliza lakini hatujui kama uamuzi wake huo atautekeleza
au vinginevyo lakini naamini Bocco akicheza tutakuwa na nafasi kubwa ya
kushinda mechi hii,” alisema mchezaji huyo.
Bocco aliyejiunga na Simba akitokea Azam FC, alikuwepo kambini
Zanzibar na Simba licha ya kusumbuliwa na jeraha la kifundo cha mguu.
Kama Omog raia wa Cameroon atamuanzisha Bocco, Simba katika safu yake ya
ushambuliaji itakuwa na Emmanuel Okwi na Bocco huku pembeni wakicheza
Shiza Kichuya na Haruna Niyonzima.
No comments:
Post a Comment