MAENEO YAPI YALITUMIKA
KUPITISHA DAWA ZA KULEVYA
Kwa mujiblu wa ripoti hii Bara la Afrika liliendelea
kutumika kupitisha dawa za kulevya. Afrika Magharibi ilitumika mara kwa mara
kupitisha Cocaine na dawa nyingine kuelekea bara la Ulaya wakati Afrika ya
Kaskazini iliendelea kuwa chanzo kikuu cha dawa zilizoingia barani Ulaya.
Kutumika kwa Afrika ya Mashariki kama kitovu cha kusafirisha heroin iliyotokea
Afghanistan ikipelekwa bara la Ulaya kuliongezeka.
Hali hii inachukuliwa kuwa ndiyo sababu ya
kuongezeka kwa matumizi ya heroin katika eneo la Afrika ya
Mashariki.Wafanyabiashara wa dawa za kulevya waliwalenga watu wenye kipato cha
kati ili kuongeza masoko ya dawa hizo katika nchi ambazo biashara hiyo ilipitia
zikiwemo za Benini na Namibia.
Ongezeko la biashara ya dawa za kulevya barani
Afrika, limeongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa vijana wadogo na
kuongeza vitendo viovu vinavyofanywa na magenge ya kihalifu. Katika eneo la
Afrika ya Magharibi na Afrika ya Kati, uhalifu wa kimtandao ulisababisha
madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa kukuza biashara ya dawa za kulevya
na kuongeza idadi ya wagonjwa wa dawa za kulevya pamoja na kusababisha wahalifu
wachache wenye silaha kuhodhi madaraka na mali nyingi.
Ingawa kumekuwepo na jitihada zinazofanywa na nchi
za magharibi mwa Afrika kupitia Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi
(Economic Community of West Africa-ECOWAS), kwa ujumla, biashara ya dawa za
kulevya na matumizi ya dawa hizi katika eneo hili yameongezeka.
Kwa mujibu wa mamlaka zinazosimamia sheria nchini
Afrika Kusini, makundi ya kusafirisha dawa za kulevya kutoka China na Eneo la
Balkan yalianzishwa katika eneo la kusini mwa Bara la Afrika huku yakijikita
katika kusafirisha heroin kupitia Maputo na kuipeleka nchini Afrika Kusini.
SHERIA, SERA NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA
NCHI ZA AFRIKA
Bara la Afrika limechukua hatua mbalimbali
kukabiliana na Tatizo la Dawa za Kulevya. Mwaka 2015 Umoja wa Afrika uliandaa
na kujadili Mkakati wa udhibiti wa dawa za kulevya unaojikita zaidi kwenye
kuzuia matumizi na kuwatibu watumiaji wa dawa hizo. Aidha, ECOWAS, iliandaa
Mpango Kazi wa Kupambana na Biashara ya Dawa za Kulevya na Uhalifu wa Kimataifa
katika nchi za Afrika Magharaibi. Nchi za Ghana, Misri na Nigeria ziliimarisha sheria
na uwezo wao wa kupambana na dawa za kulevya. Afrika Kusini iliitisha kikao
kujadili njia bora zaidi ya kukabiliana na matumizi ya bangi na utegemezi
miongoni mwa watumiaji.
No comments:
Post a Comment