![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhythDjMmTNFu9tDraIXegMhSJ5eV78VwPQ34JCuKbipVppuc0kEVH3blAH2mcUaOGiD5wYk0ESKbOgl4rXIRvWky5PTkYUVS2iiNIor5dWZDAOUKxkkAkqE2oJedbh5f8xv9CCbGTVcgyU/s400/1.jpg)
Mahakama
ya Wilaya ya Ilala imetupilia mbali pingamizi la kutopokea maelezo,
lililowekwa na upande wa utetezi kwenye kesi ndogo ndani ya ile ya
msingi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, inayomhusu Salum Njwete maarufu
Scorpion (34).
Scorpion anakabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi kwa kumtoboa macho, Said Mrisho.
Mahakama
ilifikia uamuzi huo baada ya upande wa utetezi kudai Scorpion
alishurutishwa kutoa maelezo kwa nguvu, ikiwamo kupigwa na kuteswa
katika Kituo cha Polisi Buguruni.
Akisoma
uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi, Flora Haule alisema mahakama imetupilia
mbali pingamizi hilo baada ya kubaini utetezi huo ni kinyume na hoja ya
pingamizi lililowekwa awali.
Hakimu Haule alisema kwamba maelezo ya mshtakiwa yanatia shaka kutokana na kutofautiana.
Alisema
maelezo ya awali ni kwamba alilazimishwa kutoa maelezo huku akipigwa na
kuteswa, lakini mengine anadai aliambiwa aandike ili aachiwe ndio maana
alifanya hivyo. Baada ya kutoa uamuzi huo, Koplo Bryghton wa Kituo cha
Polisi Buguruni aliendelea na ushahidi.
Scorpion
anadaiwa Septemba 6 mwaka jana saa nne usiku, maeneo ya Buguruni,
aliiba vitu mbalimbali vya Mrisho vyenye thamani ya Sh474,000 na kwamba,
kabla na baada ya kutekeleza uhalifu huo, alimchoma Mrisho sehemu
mbalimbali za mwili ikiwamo machoni, tumboni na mabegani.
No comments:
Post a Comment