MABINGWA mara moja wa zamani, Azam FC inapaswa kupandisha kiwango
chao kiufungaji msimu huu na mchezo wa raundi ya saba ugenini vs Mbao FC
unapaswa kuambatana na umakini mkubwa katika kujilinda kwani timu hiyo
ya Mwanza inapenda kushambulia sana ikicheza katika uwanja wa Kirumba.
Mbao FC japokuwa haijapata ushindi wowote katika uwanja wao wa
nyumbani lakini kiufungaji kikosi hicho cha kocha Mrundi, Etienne
kimefanikiwa kufunga magoli manne katika uwanja wa Kirumba dhidi ya
Simba SC na Mbeya City FC huku mshambulizi wake Habib Hajji akiwa tayari
ameshafunga magoli matatu kati ya nane ya timu yake.
Beki ‘yanya’ ya Mbao, wafungaji butu Azam FC
Mlinzi wa kulia, Boniphace Maganga amefunga magoli mawili hadi sasa.
Stahili yake ya kupanda kuongeza nguvu katika mashambulizi na umakini
wake katika kupiga mashuti ya mbali yenye mwelekeo sahihi ulimfanya
mlinzi huyo chipukizi wa Taifa Stars kufunga goli la ushindi wakati Mbao
FC ilipopata ushindi pekee msimu huu vs Kagera Sugar FC (ugenini).
Mlinzi wa kati na nahodha wa kikosi hicho Mrundi, Yusuph Ndikuma
amefunga goli moja na kufanya safu hiyo ya ulinzi kuwa na idadi kubwa
zaidi ya magoli ya kufunga hadi sasa wakati ligi ikiwa imeshachezwa
michezo sita kwa kila timu.
Kiuzuiaji, Mbao FC ni timu ya tatu iliyoruhusu magoli mengi katika
ligi msimu huu (imefungwa magoli tisa.) Wakati safu hiyo ya ulinzi ya
kikosi cha Etienne ikiruhusu magoli tisa, safu ya mashambulizi ya kikosi
cha Mromania, Aristica imefunga magoli matano tu.
Mbaraka Yusuph ndiye kinara wa ufungaji wa Azam FC hadi sasa akiwa
amefunga magoli mawili. Mghana, Yahaya Mohamed amefunga goli moja sawa
na kijana Peter Paul ambaye alifunga goli la kusawazisha wakati Azam FC
ilipolazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Singida United. Huku nahodha wa
kikosi, Himid Mao akifunga katika sare iliyopita Mwadui FC 1-1 Azam FC.
Kitendo cha washambuliaji hao kufunga magoli manne katika michezo
sita kwa timu inayojengwa bado nasisitiza wako katika mwendo mzuri na
kwa kutumia udhaifu wa Mbao FC katika kujilinda kikosi hicho kilichotwaa
ubingwa msimu wa 2013/14 kinaweza ‘kunoa’ makali zaidi kwa kufunga
walau magioli mawili katika mchezo mmoja kwa mara ya kwanza msimu huu.
Mbio za ubingwa ni sasa
Kuwa na pointi 12 sawa na viongozi wa ligi Simba SC, MtIbwa Sugar na
mabingwa watetezi kunaonyesha kuwa ligi bado ‘mbichi’ nab ado hakuna
tofauti kubwa kati ya timu na timu.
Kwa Azam FC ambao walianza maandalizi yao Juni na kuwa timu ya kwanza
kufanya hivyo sasa wanapaswa kuanza kufunga kweli ili kuthibisha kuwa
wako tayari kwa mbio za ubingwa na pengine kushinda taji hilo kwa mara
ya pili mwishoni mwa msimu.
Kushindwa kupata matokeo ya ushindi katika michezo vs Singida United (
Jamhuri Stadium, Dodoma) na Mwadui FC (Mwadui Complex) bado hakupaswi
kuwakatisha tama kwani wamekutana na timu ambazo pengine zingiweza
kuwafunga bila Azam FC kukomboa goli katika kila mchezo.
Ila timu yenye dhamira ya ubingwa inapaswa kushinda walau mchezo
mmoja na kutoa sare mbili katika viwanja vya ugenini. Lakini bahati
mbaya kwa Azam FC wanaweza kushindwa kupata ushindi katika mchezo wa
tatu mfululizo wakicheza ugenini kwa sababu wanakutana na Mbao ambao pia
wanasaka ushindi wa kwanza nyumbani msimu huu.
Kumbuka Mbao FC nao wanaingia katika mchezo huu vs Azam FC Jumamosi
hii wakipambana kuepeka sare ya tatu mfululizo katika uwanja wa
nyumbani. Nani mshindi?
No comments:
Post a Comment