![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjdsmiFS6JRC7YQFu9h2fFtb3XJbm4XzQCsWqcJQw8OpeZjONKIWB_B9Ub1jTkdwJlsYkIe0XgdXPyUQ3_-4bS_Mw9adZvDRf2aYQDNTAAR_-5B_F973G8fw8E4ouo9orIgHsmFv8h_kUJI/s400/1.jpg)
Wakati
mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu akieleza kuwa
anakusudia kuwasilisha hoja ya muswada binafsi kwa Spika utakaoweka
sharti la kurejea upya mjadala wa Katiba mpya, utafiti umeonyesha kuwa
wananchi wawili kati ya watatu wanasema Tanzania inahitaji Katiba mpya.
Pia, nusu ya wananchi wanasema mchakato wa Katiba uanze upya na tume mpya.
Jana kupitia katika akaunti zake za mitandao ya kijamii ya Instagram, Twitter na Facebook Nyalandu aliandika, “Nakusudia
kuwasilisha kwa Spika wa Bunge, mheshimiwa Job Ndugai azma yangu ya
kuleta muswada binafsi wa sheria katika kikao kijacho cha Bunge
itakayoweka sharti la kurejea upya mjadala wa Katiba mpya ya Tanzania,
kwa kuzingatia rasimu ya Katiba ilivyowasilishwa na Tume ya Jaji
Warioba.”
Nyalandu alisema muswada huo anatarajia kuuwasilisha kwenye kikao kijacho cha Bunge.
Akizungumza
kwa simu baada ya kuandika maneno hayo, Nyalandu alisema amekusudia
kupeleka muswada huo kwa sababu mchakato wa Katiba mpya haukufikia
mwisho.
“Nitafurahi
sana kama jambo hili litafanikiwa kwa kuwa lina umuhimu wake kwa kila
mtu. Suala hili pia halina itikadi za vyama vya siasa na lina masilahi,
kwa sababu Katiba ina uwezo wa kukaa zaidi ya miaka 100,” alieleza
Nyalandu.
Mbali
na Nyalandu kueleza hayo, mwezi uliopita asasi za kiraia zaidi ya 80
zilijitokeza hadharani na kutoa tamko zikisema kwamba huu ni wakati
mwafaka wa mchakato wa Katiba kuanza upya ili ifikapo 2020 iwe
imepatikana.
Kabla
ya asasi hizo kutoa tamko, Jukwaa la Katiba lilijitokeza na kusema
litaandaa maandamano ya amani kumueleza Rais John Magufuli umuhimu wa
kuandika Katiba mpya.
Mbali
na hayo, jana matokeo yaliyotolewa na Twaweza katika utafiti uitwao
‘Zege imelala?’ yameeleza kuwa wananchi wawili kati ya watatu wanasema
Tanzania inahitaji Katiba mpya, huku nusu yao wakisema mchakato wa
Katiba uanze upya na tume mpya.
Utafiti
huo umesema muhtasari unatokana na takwimu kutoka sauti za wananchi
ukiwa ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa
unaotumia simu za mikononi.
Mkurugenzi
mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema, “Wananchi wanataka Katiba
mpya. Wengi wao wanataka mchakato uanze upya na tume mpya katika ukurasa
mpya. Hata hivyo, wapo wananchi ambao wapo tayari kusonga mbele kwa
kutumia rasimu iliyoandaliwa na tume iliyotangulia.”
Pia,
alisema kuwa wananchi wanaunga mkono kipengele kilichoongeza madaraka
ya Bunge katika suala la kuwapitisha mawaziri walioteuliwa na
kinachowapa wananchi haki ya kuwaondoa wabunge wanaozembea kazini.
Eyakuze alisema utafiti umedhihirisha uwajibikaji wa siasa kwenye uhalali wa mchakato wa Katiba.
“Matokeo
yameonyesha dhahiri kwamba wananchi wengi wanatatizwa katika
kutofautisha kitendo cha Ukawa kugomea Bunge la Katiba na migomo
mingineyo. Ushabiki wa kisiasa huwafanya watu wengi kutozingatia uhalali
wa jambo husika,” alisema.
Eyakuze
alisema, “Hivyo basi; vyovyote tutakavyofufua mchakato wa Katiba ni
muhimu kwa wahusika wakuu kuheshimu na kutambua kwamba sheria mama ya
nchi ni ya thamani zaidi kuliko tofauti za kisiasa. Tanzania inahitaji
mchakato wa Katiba utakaozingatia uhalali na ujumuishi wa Watanzania
wote.”
Taarifa
ya Twaweza kwa vyombo vya habari ilisema asilimia 67 ya Watanzania
wanasema ni muhimu kwa Tanzania kupata Katiba mpya na asilimia 56
wanasema toleo la mwisho la rasimu ya Katiba lipigiwe kura na wananchi.
Hata hivyo, asilimia 48 ya wananchi wanasema kwa maoni yao, Katiba mpya haitapatikana ndani ya miaka mitatu ijayo.
Taarifa
hiyo ilisema wananchi wanaendelea kuunga mkono kwa nguvu kubwa uundwaji
wa Katiba mpya inayotilia mkazo suala la uwajibikaji.
Ilisema
asilimia 79 wanataka mawaziri wanaoteuliwa wapitishwe na Bunge na
asilimia 64 wanataka wawe na uwezo wa kuwaondoa wabunge katikati ya
mihula yao iwapo hawatatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hata
hivyo, wananchi wamegawanyika kwenye baadhi ya hatua za uwajibikaji
zilizopendekezwa ikiwamo kuzuia viongozi na watumishi wa umma kuwa na
akaunti nje ya nchi (asilimia 52 wanaunga mkono), kuwapo kwa ukomo wa
ubunge (asilimia 52 wanaunga mkono) na kuweka kanuni za uwazi na
uwajibikaji kuwa sehemu ya tunu za Taifa (asilimia 48 wanaunga mkono).
Hivyo vyote ni vipengele vya rasimu ya Katiba ambavyo viliondolewa na Bunge Maalumu la Katiba.
Twaweza
ilisema wananchi pia wanaunga mkono kuondolewa kwa kipengele
kinachotaka kuchunguza na kudhibiti ofisi ya Rais (asilimia 55) na
mawaziri kuchaguliwa kutoka nje ya Bunge (asilimia 62).
Matokeo
hayo taasisi hiyo imesema yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka
kwa wahojiwa 1,745 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar
haihusiki kwenye utafiti huu) Juni hadi Julai 2017.
Kuhusu
muundo wa Serikali ni moja kati ya vipengele vilivyoibua mjadala mzito
wakati wa mchakato wa kuunda Katiba mpya na hatimaye kuwagawa wananchi.
Asilimia 42 ya wananchi wa Tanzania Bara waliunga mkono muundo wa
Serikali mbili.
Twaweza
imesema muundo wa Serikali moja ulikubalika kwa asilimia 25 na ule wa
Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulipendwa
na asilimia 16.
Mchakato wa Katiba mpya ulisimama Oktoba 2014 baada ya Tume ya Uchaguzi kudai kuwa ungeiliana na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
No comments:
Post a Comment