Nyasi
bandia za Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam zinatarajiwa kutimbika
kwa mchezo wa watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
Jumamosi kuanzia Saa 10:00 jioni.
Na
wakati kikosi cha Yanga kikiwa njiani kurejea Dar es Salaam kutoka
Shinyanga ambako Jumapili walishinda 4-0 katika mchezo mwingine wa Ligi
Kuu dhidi ya wenyeji, Stand United, Kamusoko, Ngoma na Tambwe waliokuwa
majeruhi wanatarajiwa kuungana na wenzao leo.
Watatu
hao hawakusafiri na timu wiki iliyopita kwa mechi za Kanda ya Ziwa
kutokana na kuwa majeruhi, lakini akizungumza leo, Msemaji wa Yanga, Dissmas Ten amesema kwamba wachezaji hao
wataungana na wenzao leo.
“Ngoma,
Kamusoko na Tambwe tayari wote wako fiti na wamekuwa wakifanya mazoezi
kwa wiki sasa. Matarajio ni watajiunga na timu leo kwa mazoezi ya siku
tatu zilizobaki kabla ya mechi na Simba,”amesema Ten.
Pamoja
na kuwakosa wachezaji wake hao nyota watatu kwa muda mrefu, lakini
imemudu kwenda sawa na mahasimu wao, Simba katika mbio za ubingwa.
Simba,
Yanga pamoja na Mtibwa Sugar zote zinalingana kwa pointi hivi sasa,
kila moja ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba na mshindi wa
Jumamosi atatanua kwapa kileleni, wakati sare inaweza kuwashusha wote,
iwapo Wakata Miwa wa Manungu watashinda dhidi ya Singida United
Jumapili.
No comments:
Post a Comment